Chuo Kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuehne Foundation ya Uswizi (switzerland) chini ya mradi wa "Logistics Education for Emerging and Developing Countries (LEED)" wametoa mafunzo kwa wadau mbalimbali wa usafiri na usafirishaji ili kuhakikisha usafiri wa mjini unakuwa endelevu, wa uhakika, salama na wa haraka kwa wananchi.
 
Akifungua mafunzo hayo Machi 26, 2024, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Dkt. Coretha Komba amesema mafunzo hayo yamelenga kuwafikia wadau wa usafiri na usafirishaji ili huduma hiyo iweze kuboreshwa kwa kuondoa au kupunguza changamoto mbalimbali za huduma hiyo. Mradi huu wa LEED umekuja na njia za kiteknolojia za kuleta ufumbuzi wa changamoto ya usafiri katika maeneo ya mijini.
 
Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa huo na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Omary Swalehe, amesema kuwa lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki kuhusiana na changamoto za usafiri mijini pamoja na kupata ufumbuzi wa changamoto katika usafiri ili kuleta ahueni kwa wasafiri na wasafirishaji.
Dkt. Omary amesema kuwa changamoto za usafiri mijini hazitatuliwa na Serikali peke yake bali kwa kushirikisha sekta binafsi pamoja na watumiaji ili kuhakikisha usafiri mijini unakuwa salama, wa uhakika na wa haraka.
 
"Kuondoa changamoto za usafiri mjini ni suala pana, ndio maana tumealika wadau mbalimbali, lengo ni kuwa na uelewa wa pamoja kwa sababu changamoto hizi haziondolewi na Serikali pekee yake bali kwa kushikiana na wadau hususan watumiaji". Dkt Swalehe alisisitiza.
Kwa Upande wa mwakilishi wa wanaopewa mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo hayo yatakwenda kuwasaidia kutafuta njia rahisi ya kurahisisha usafiri mijini bila kutumia muda mwingi wala nishati kubwa bila kuathiri mazingira.
 
Mafunzo hayo yamehusisha Wahadhiri wa masuala ya usafirishaji, wanavyuo wanaosoma masuala ya usafirishaji, wadau kutoka halmashauri za wilaya za mijini pamoja na wadau kutoka taasisi binafsi za masuala ya usafirishaji.
 

 

 

Mzumbe University,
P.O Box 1 Mzumbe,
Morogoro, Tanzania.
Tel: 255 (0) 23 2931220/1/2
Fax: 255 (0) 23 2931216
Cell: 255 (0) 754694029
Email: .
Go to top