CHUO KIKUU MZUMBE CHAENDELEA KUBORESHA MBINU ZA UTENGENEZAJI MAUDHUI NA UFUNDISHAJI KWA NJIA YA MTANDAO

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ‘HEET’ kimeandaa warsha ya siku tatu kuhusu utengenezaji wa Maudhui ya Kozi, Ujifunzaji Mseto na Ujifunzaji kwa Njia ya Mtandao inayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 06 - 08 Januari 2025.

Akifungua warsha hiyo kwa niaba ya Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Dkt. Coretha Komba amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo ni vema kutumia teknolojia iliyopo katika kurahisisha ufundishaji kwani suala la kujifunza au kufundisha kwa njia ya mtandao haliepukiki katika karne ya sasa.

Kwa upande mwingine, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui aliwajuza washiriki wa warsha hiyo kuwa madhumuni ya Mradi wa HEET ni kuongeza idadi kubwa ya wanafunzi watakaojiunga na Chuo, kuboresha mitaala ya ufundishaji itakayowajengea wahitimu uwezo wa kufikia viwango vya soko la ajira ili kuweze kujiajiri na kuajirika.

Akiwasilisha mada, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Maktaba Dkt. Kardo Mwilongo amesisitiza kuhusu machapisho huria ya kielektroniki kwa kuainisha kuwa ndio yanayotoa dira sahihi ya matumizi ya huduma ya kufundishia wanafunzi huku akiwaonyesha wanataaluma hao kwa vitendo namna ya kuandaa machapisho huria ya Kielektroniki. Aidha, Dkt. Kardo amesisitiza walimu na wanafunzi kutumia machapisho hayo kwa kiwango cha juu katika nyakati hizi za ujifunzaji mseto.

Naye, Kaimu Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa TEHAMA Dkt. Perpetua Kalimasi amesema kuwa ni vizuri kila mwanataaluma kubadili mtazamo wa kufundisha kwa njia za kizamani zinazomtaka mwalimu kuwepo darasani na wanafunzi muda wote na kuanza kufundisha kwa njia za kimtandaoni. Amesema njia hii itasaidia kuwafikia wanafunzi wengi nje ya Chuo. Ili kufanikisha suala hilo, Dkt. Kalimasi alisema kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimeboresha miundombinu mbalimbali vya TEHAMA chuoni ikiwemo kukamilisha ofisi za "Multimedia" ambazo zina vifaa vya kisasa vya ki-KITEHAMA vya kumsaidia mwalimu kurekodi vipindi vya kufundishia wanafunzi mtandaoni (online).

***************

 

 

Contact Us

Vice Chancellor,

Mzumbe University,

P.O.BOX 1,

Mzumbe, Morogoro.


Tel: +255 023 2604380/1/3/4
Fax: +255 023 2931216
Cell: +255 0754 694029
Email: This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.